MSOL AB MUSIC STUDIO OF LEARNING

MSOL AB - MUSIC STUDIO OF LEARNING OF SWEDEN Kuanza | MSOL AB | Huduma | Wasanii | Video na muziki | Film | Mgeni Msanii | Mawasiliano | IN ENGLISH


Kuhusu sisi

Mimi naitwa Peters Mhoja, mwanzilishi na Chief Executive Officer (CEO) wa Kampuni ya Music Studio Of Learning Of Sweden AB. Ni msukuma wa Shinyanga-Tanzania. Kwa sasa familia yetu yote (ukoo) wanaishi Kahama-Shinyanga. Mimi ninaishi Sweden. Historia yangu kikazi kwa kifupi ni kama ifuatayo. Tangu mwaka 1975 nimefanya kazi kama fundi East African Posts & Telecommunications baadaye ikaitwa Tanzania Posts & Telecommunications na baadaye serikalini. Niliondoka Tanzania tarehe 8 septemba 1980 kwenda kusoma masomo ya juu(Electrical Engineering-Electronics) Urusi hadi mwishoni mwaka 1989 nilipopata nafasi ya kazi Sweden.

Nilikuja Sweden tarehe 6 februari, 1990 baada ya kupata makaratasi yangu yote muhimu ya kibali cha kuishi na kufanya kazi kama fundi katika Kampuni ya Ericsson idara ya Radio Base Station (RBS). Ili kupata nafasi ya kufanya kazi pasipokuwekewa aina fulani ya mipaka katika kazi yangu ilikuwa ni vema kuchukua uraia wa Sweden. Nilifanya hivyo.

Mwaka 2010 Kampuni ya Ericsson-Gävle nilipokuwa nikifanya kazi, iliamua kuhamisha kazi zake zote kwenda nchi nyingine ya nje ya Sweden. Wafanyakazi wote tulipewa nafasi ya kuchagua. Kwenda kuendelea kufanya kazi mji mwingine Sweden au kuacha kazi kwa hiari na ukiamua kuacha kwa hiari tulitakiwa kufanya kazi hadi tarehe 31 desemba, 2011. Niliamua kuacha kazi kwa hiari ili nifanye kitu ambacho roho yangu ilikuwa ikiniambia nifanye kwa miaka mingi. Nilikuwa na hamu kubwa sana ya kufanya kitu kwa kutumia elimu yangu na utaalamu wa kifundi nilioupata Ulaya niupeleke Tanzania. Niliona kitu ambacho naweza kukifanya ni kuanzisha kampuni ambayo itakuwa ya manufaa kwa Watanzania wengi zaidi. Fursa niliyoiona ya kuwapa ni hii ya kuwatengenezea studio ya kufanyia kazi zao Ulaya na kuwapa nafasi ya kuwatumia nguli wa muziki/filamu wa Ulaya na duniani na kubadirishana nao elimu na utalaam wa kila mmoja "live". Nikaanza kuiunda Kampuni ya Music Studio Of Learning Of Sweden AB.

Tangu nikiwa kijana mdogo nilipenda sana muziki. Miaka ya 1970, nilikuwa choirmaster wa Uchama Upper Primary School-Nzega na mcheza maigizo. Mwaka 1974 wakati nikisoma Dar es salaam Technical College nilijiunga na bendi ya muziki iliyokuwa ikiitwa Tanzania Jazz Band-Mtaa wa Livingstone Dar es salaam iliyokuwa mali ya Mzee Bayuni nikiwa mwimbaji.

Mwaka 1978 kwa muda maalum nilipata nafasi ya kufanya kazi RTD.

Nilipokuwa nikifanya kazi hizo za kifundi RTD-Pugu road na watalaam kutoka Sweden tuki-install mitambo ya Toresimu nilipata nafasi ya kuwaona mafundi mitambo wa RTD wakirekodi bendi mbali mbali zilizokuwa zinakuja kurekodi nyimbo za kuhamasisha katika mapambano yetu na Nduli Idd Amin 1978 na 1979. Hadi leo hii kitu hicho kilibaki kichwani mwangu. Kuianzisha MSOL sio kwa bahati mbaya kuna historia yake kamili katika maisha yangu.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikizifuatilia kwa ukaribu bendi zetu na wanamiziki wake wanavyoishi maisha duni na wanapoondoka duniani kila kitu katika bendi huishia hapo. Nilipata kuiangalia filamu ya kwanza ya Kitanzania Fimbo ya Mnyonge. Ilikuwa filamu nzuri sana kwani Msanii Yombayomba aliicheza kiuhalisia wa Kitanzania kabisa. Lakini baada ya kuharibika mkanda huo ndiyo ukawa mwisho wa filamu hiyo. Hadi leo hii hakuna anayejua kuwa tuliwahi kuwa na filamu yetu na wala hakuna mtu anayemfahamu msanii wetu Yombayomba wala hatujui kama yuhai ama la.Kuna wasanii wetu wa michezo ya redio kama vile Pwagu na Pwaguzi, Ramadhani Mwanahewa, Mzee Jongo na wengine wengi, hakuna anayewakumbuka. Wasanii wa Bongomovie wanapokusanyika katika kuenzi wasanii wenzao kama vile Kanumba, wawakumbuke pia wasanii wa zamani, hao ndiyo Wazazi wao katika kazi zao.

Hali ni ile ile kwa muziki na wanamiziki wetu. Sio Tanzania pekee ni vivyo hivyo katika baadhi ya nchi zingine Afrika. MSOL itajitahidi kwa kutumia utaalam wa kisasa na kwa kuwatumia vyema wataalamu wake, kufanya kama wafanyavyo katika nchi zilizoendelea kuzitunza na kulinda kazi zote za wasanii kwa wale watakaokuwa wateja wake. Fedha zitakazokuwa zikipatikana katika mauzo ya kazi zote zitawakilishwa kwa wahusika ama ndugu kama atakavyoelekeza msanii mwenyewe na kutoa mawasiliano kamili maisha yote.

Katika kutaka kuelewa jinsi itakavyofanya kazi MSOL-AB kwa ufanisi na kufikia lengo nililolifikiria. MSOL-AB tulijikita zaidi katika utafiti wetu kwa kuwahoji Wataalamu wa muziki na kushiriki majadiliano ya pamoja nao, na pia mimi nilijadiliana mambo kama hayo na Wasambazaji wa miziki duniani. Nimefanikiwa kutengeneza "network" kubwa na Wasambazaji hao. Na ilikuwa ni kupata mbinu za kuwaendeleza Wanamuziki wa Tanzania (Tanzania Kwanza) wenye viwango mbalimbali vya elimu, na niliendelea kufanya utafiti wa kina na Wasambazaji hao ili kuelewa sababu zinazoifanya miziki ya Tanzania kutokuingia katika soko la dunia. Nilikuja kuelewa kuwa miziki yetu ni mikondefu na ina matobo mengi, haihusiani kabisa na lugha. Muziki una lugha yake duniani. Ili kujiweka katika hali ya uhakika na kile nilichoelezwa na Wasambazaji, nilichukua kozi katika Chuo Kikuu cha Muziki duniani Stockholm SAE Institute. Nilichukua kozi ya "Electronic Music Production"- Nikaona kuwa miziki yetu mingi imerekodiwa na ku-miksiwa hata mastering yake vyote viko katika viwango vya chini sana. Ili muziki wetu usikike katika masikio ya watu duniani,tunahitaji kujaza matobo yaliyomo katika miziki yetu ili inenepe katika kufikia kiwango cha kusikilizwa.
MSOL-AB ni Kampuni itakayokuwa ya Mataifa yote duniani kama tulivyokusudia. Hatutabadirisha kitu katika muziki wa mtu yeyote. Muziki utabaki ni ule ule kwa mfano wa Kitanzania, uwe Bongo Fleva, Hipop, Gospel, Dansi ama Taarab. Wakati wote tutayathamini maoni ya mwanamuziki mwenyewe kadri atakavyopendekeza muziki wake uwe. Mimi kama Mkurugenzi Mkuu wa MSOL-AB, nitafurahi nikipata ushirikiano wa karibu wa BASATA na COSOTA. Nia ni kuviinua viwango vya miziki na filamu zetu. Nitakuwa nikiiboresha kila kitu nitakapokutana na aina zote za changamoto hadi nihakikishe kuwa miziki na filamu za Tanzania zinapata soko duniani.

Peters Mhoja / CEO / MSOL - AB

MSOL AB - MUSIC STUDIO OF LEARNING OF SWEDEN

Kujiunga na sisi kwenye facebook.

Admin >>